Abstract:
Makala haya yamejadili matumizi ya uhalisia mazingaombwe kama mbinu ya mtindo wa uandishi wa
ubaadausasa katika riwaya ya Nyuso za Mwanamke (2010) ya S. A. Riwaya hii imedhihirisha upya kwa
kukaidi mtindo wa uandishi wa kimapokeo ukiojikita katika uhalisia, na kugeukia mtindo wa uandishi wa
kibaadausasa. Makala haya yanachunguza matumizi ya uhalisia mazingaombwe katika riwaya hii, kama
kipengele mojawapo cha mtindo wa uandishi wa ubaadausasa. Lengo kuu la makala haya ni kubainisha
vipengele vya uhalisia mazingaombwe na namna vimetumika katika riwaya ya Nyuso za Mwanamke. Makala
haya yameongozwa na Nadharia ya Ubaadausasa inayopendekeza uanuwai wa mawazo kwa kukaidi kuwepo
na mtazamo mmoja wa kueleza tajriba tofauti za binadamu, au simulizi kuu. Sampuli dhamirifu ilitumika
kuteua riwaya ya hii. Data ilipatikana kupitia usomaji wa kina wa riwaya. Data ilichanganuliwa kwa
kuzingatia mihimili ya Nadharia ya Ubaadausasa na kuwasilishwa kwa maelezo ya kinathari. Matokeo
yalibainisha kwamba riwaya hii iliziba mipaka kati ya uhalisia na umazingaombwe kupitia matumizi ya
wahusika binadamu wenye nguvu za ajabu kama vile kuwasoma watu. Aidha, riwaya hii ilitumia viumbe wa
ajabu kama vile mizuka, vivuli, majini na wafu kuwakilisha hali halisi ya dunia ya sasa ambayo imejaa
mambo mengi ya ajabu yasiyoelezeka. Katika kutamatisha, ilibainika kuwa matumizi ya uhalisia
mazingaombwe ni mbinu ya kiumbuji anayotumiwa mwandishi kukaidi simulizi kuu ya uandishi wa
kimapokeo wa riwaya ya Kiswahili uliojikita katika uhalisia. Matumizi ya mtindo huu ni dhihirisho la
mabadiliko katika uandishi wa riwaya ya Kiswahili.