Abstract:
Makala haya yanachanganua suala la changamoto zinazokabili umiliki na matumizi ya
ardhi barani Afrika kama lilivyosawiriwa katika riwaya za karne ya ishirini na moja, kwa
kurejelea riwaya za Chozi la Heri (2014), Msimu wa Vipepeo (2009) na Nakuruto (2006).
Ardhi ni miongoni mwa rasilimali muhimu katika maisha ya binadamu hasa katika
uzalishaji mali. Huwa chanzo cha mahitaji ya kimsingi kama vile chakula na makaazi.
Aidha, uwezo wa kumiliki ardhi huwa ni sifa kuu ya maendeleo na mabadiliko mengi
katika jamii ambayo yamewahi kushuhudiwa duniani. Tungo za kifasihi tulizoziteua
kimakusudi zilifanikisha utafiti huu kwa sababu fasihi huwa imefungamanishwa
kibunifu na maisha halisi ya binadamu. Sifa kuu ya riwaya hizi ni kwamba zimeliangazia
suala la ardhi kwa mapana. Isitoshe, zimetungwa katika kipindi cha karne ya ishirini na
moja ambacho utandawazi umeenea na kuimarika barani Afrika. Ili kufanikisha udurusu
huu, tuliligawa suala letu la utafiti katika sehemu tatu kuu: kipindi cha kabla ya ukoloni,
kipindi cha ukoloni na kipindi cha utandawazi. Uchanganuzi matini huu wa kimaktaba
uliongozwa na nadharia ya Baada-ukoloni. Umuhimu wa makala haya unatarajiwa kuwa
pamoja na kudhihirisha mitazamo ya watunzi mbalimbali kuhusu changamoto katika
umiliki na matumizi ya ardhi barani Afrika; pamoja na mapendekezo ya namna za
kuzitatua. Tunatarajia kutoa mchango wa kitaaluma kuhusiana na suala hili hivyo
kuwafaa watafiti wa baadaye na watunga sera zinazohusiana na suala la umiliki na
matumizi ya ardhi barani Afrika.