Abstract:
Madhumni ya makala haya yalikuwa ni kubainisha na kuchanganua mitazamo
ya WaKenya kuhusu Tangaavu la Korona (COVID-19) kama inavyodhihirika
kupitia mazungumzo ya kikawaida, Skaz. Hii ni kutokana na ukweli kwamba,
tafiti za awali kuhusu mada hii hazikukitwa katika misingi ya Skaz. Kwa hivyo,
taarifa nyingi kuhusu Tangaavu la Korona zilizowasilishwa na Shirika la Afya
Ulimwenguni pamoja na Wizara ya Afya nchini Kenya zilikuwa za kitaalamu
(kiakademia). Utafiti huu ulikuwa wa nyanjani na ulifanyika Kericho, Kenya.
Mtafiti aliteua sampuli kimakusudi na kukusanya data kwa kutumia mbinu ya
utazamaji nyanjani. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni ya Usemezano
ikijumuisha sifa za Skaz kama ilivyoelezwa na Bakhtin ikitiliwa nguvu na
Mbinu ya Urazini wa Kiwatu kama ilivyoendelezwa na Sacks na wenzake.
Uchanganuzi wa data ulionesha kuwa, mwanzomwanzo, kutokana na kukosa
ufahamu wa kitaaluma kuhusu ugonjwa “mpya” Tangaavu la COVID-19 kwa
jumla, bila kukusudia kupotosha WaKenya waliibuka na mitazamo mbalimbali
kuhusu ugonjwa huu. Mitazamo hii pia ilitokana na jitihada za hekaheka kutafuta
njia za kuzuia usambazaji na hata tiba miongoni mwa wanajamii. Utafiti huu
umeweka wazi mitazamo “hasi” kuhusu ugonjwa wa COVID-19 jinsi
ili(na)vyodhihirika katika mazungumzo ya kikawaida na hivyo kuwafaidi
watafiti wa utabibu na wapangaji sera za kiserikali kutilia maanani mitazamo
katika lugha ya kikawaida haswa kwenye majanga ya kiulimwengu.