Abstract:
Makala haya yanakariri hoja kwamba ushairi wa Wagunduzi ni ushairi wa
Wanajadi. Mapitiyo yetu ya maandishi yanayozungumziya ushairi wa
Kiswahili yameonesha kwamba kuna makundi mawili: Wanajadi, akiwamo
Sheikh Nabhany, na Wagunduzi, akiwamo Kezilahabi. Yaliyoandikwa
yanaonesha kuwa mgogoro ulizuka kutokana na wanajadi kudai kuwa ushairi
wa wagunduzi si wa Kiswahili kwa sababu haufwati urari wa vina na mizani
na hivo umbo lake ni tafauti na la mashairi ya Kiswahili. Fauka ya hayo,
wachanganuzi wa mashairi ya Kiswahili wana maoni kwamba mashairi ya
Kezilahabi ni aina mpya ya mashairi ya Kiswahili. Lengo la makala haya ni
kugeuza mwendelezo wa fikira hii. Lengo hili limefikiwa kwa kutumiya
uainishaji wa mashairi ya Kiswahili uliyotolewa na Mwanajadi Nabhany
kwamba umbo la shairi linatokana na mpangiliyo maalumu wa sauti. Kwa
kuchanganuwa umbo la shairi moja la Kezilahabi kupitiya kigezo cha bahari
ya utumbuizo, ambayo Nabhany ameiorodhesha kuwa bahari mojawapo ya
mashairi ya kijadi ya Kiswahili, tumeona kwamba ushairi wa Kezilahabi una
sifa zote, ama karibu zote, za bahari hiyo. Kwa sababu hiyo, tunahitimisha
kuwa ushairi wa Kezilahabi ni ushairi wa Wanajadi.