Abstract:
Makala haya yanatathmini uwasilishaji wa wahusika wa kimazingaombwe na
uhusika katika kazi za Kiswahili. Uchanganuzi huu ni wa kimaktaba
tukizingatia mihimili ya nadharia ya Umazingaombwe. Riwaya za Babu
Alipofufuka na Watu wa Gehenna zilichaguliwa kimakusudi kwa sababu
uwasilishaji umechochewa na mbinu ajabuajabu za waandishi katika uhusika
na usawirishaji wa wahusika kwa njia unaojenga dhamira ya
kimazingaombwe. Uwasilishaji huu unazua utata kwa wasomaji katika kunata
ujumbe unaowasilishwa na wahusika hao katika riwaya hizi teule za
kimajaribio. Waandishi hawa, Wamitia na Olali, wanasukanisha uhalisia
uliochongwa kwa njia maalum katika ruwaza inayobadilikabadilika daima,
huku wakiwakilisha matukio ya kawaida na maelezo ya kina sambamba na
vipengee vya kifantasia na kindoto na kwa kutumia mambo yaliyotokana na
visasili na hekaya. Aidha, kazi hii ilidhamiria kuthibitisha uwasilishaji wa
kiuhalisajabu katika mandari au mazingira ya kimazingaombwe. Utafiti huu
umejaribu kujaliza mapengo yanayoleta matatizo ya ufahamu na usadikifu wa
kazi tulizo teua za kihalisiajabu. Maandishi katika utafiti huu yanadhamiria
kukuza na kupanua uelewekaji wa riwaya za kisasa mbali na kufaidi wasomaji
mbalimbali na hata kuwapa motisha wahakiki kushughulikia zaidi wahusika,
uhusika na uwasilishaji katika misingi ya umazingaombwe katika fasihi
simulizi.